BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
TIMU ya Simba imeanza ligi kwa kishindo  baada ya kuibuka na ushindi wa magoli 3-1 dhidi ya Ndanda FC katika mchezo wa ufunguzi wa ligi kuu ya Vodacom uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba walianza mchezo huo kwa kasi ambapo dakika ya tatu mshambuliaji Laudit Mavugo alipiga shuti kali langoni mwa Ndanda lakini kipa Jackson Chove aliokoa na kuwa kona.

Mavugo aliipatia Simba goli la kuongoza dakika ya 19 akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na beki Mohamed Hussein kushindwa kuokolewa na mabeki wa Ndanda.

Omari Mponda aliisawazishia Ndanda kwa kichwa dakika ya 36 baada ya kupokea mpira wa adhabu uliopigwa na beki Paulo Ngalema na wachezaji wa Simba kushindwa kuokoa hatari hiyo.

Kipindi cha pili Simba waliendelea kulisakama lango la Ndanda ambapo dakika ya 73 Frederick Blagnon aliwapatia Wekundu hao goli la pili baada ya kumalizia kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Hussein.

Dakika ya 79 Shiza Kichuya alifunga goli la 'kideoni' kwa shuti kali  kufutia mpira wa kona uliopigwa na Hussein kupanguliwa na Chove kisha kumkuta mfungaji.

Simba iliwatoa Ibrahim Ajib, Jamal Mnyate na Kichuya nafasi zao zikachukuliwa na Blagnon, Mwinyi Kazimoto na Mohamed Ibrahim.

Kwa upande wao Ndanda waliwatoa Azizi Sibo na Shija Mkina nafasi zao zikichukuliwa na Bakari Mtama na Nassor Kapama.

Katika michezo mingine Mtibwa amefungwa bao 1-0 na wageni wa ligi hiyo Ruvu Shooting, Mbao wametoka suluhu na Stand United huku mchezo kati ya Majimaji na Prisons ukiendelea maafande wakiongoza kwa bao moja.

Post a Comment

 
Top