BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
TIMU ya Simba imepunguzwa kasi baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na Maafande wa JKT Ruvu katika muendelezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo ulianza taratibu huku timu zote zikishambuliana kwa zamu ambapo dakika ya 16 Atupele Green alipoteza nafasi ya wazi ya kufunga baada ya mlinda mlango Vicent Angban kutoka katika eneo lake kabla ya beki Novaty Lufunga kuokoa.

Dakika tano baadae Simba walifanya shambulizi kali langoni mwa Ruvu ambapo mpira uliopigwa na Shiza Kichuya ulipanguliwa na kipa Said Kipao na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Dakika ya 25 Nahodha wa Ruvu Michael Aidan alitolewa nje kwa machela baada ya kuumia kufuatia kugongana na mchezaji wa Simba na nafasi yake ikachukuliwa na James Msuva.

Simba waliendelea kulishambulia lango la Ruvu ambapo Kipao alifanya kazi ya ziada kuokoa mpira uliokuwa ukielekea kimiani uliopigwa kiufundi na Ibrahim Ajib dakika ya 69.

Maafande hao ambao ndiyo walikuwa wenyeji wa mchezo huo walikuwa wakianguka chini mara kwa mara hasa kipindi cha pili hali iliyoonesha kupunguza kasi ya mashambulizi ya Simba.

Ruvu iliwatoa Msuva na Ismail Amour nafasi zao zikachukuliwa na Nashon Naftari pamoja na Madenge Ramadhani. Simba iliwatoa Fredrick Blagnon, Lufunga na Jamal Mnyate wakawaingiza Ajib, Juuko Murshid na Mwinyi Kazimoto.

Post a Comment

 
Top