BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
TIMU ya Simba imelazimishwa sare ya goli 1-1 na URA toka nchini Uganda katika mechi ya kirafiki maalum kwa ajili ya kumuaga aliyekuwa nahodha wao Mussa Mgosi ambaye ameteuliwa kuwa Meneja wa klabu hiyo. Mchezo huo ulifanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

URA ndiyo walikuwa wa kwanza kupata goli dakika ya 19 kupitia kwa Nkungwa Elkanah baada ya kupokea krosi safi upande wa kushoto iliyopigwa na Sekito Sam kutokana na uzembe wa mabeki wa Simba.

Dakika kumi baadae nahodha Jonas Mkude aliisawazishia Simba kwa kichwa baada ya mpira wa adhabu uliopigwa kwa ufundi na beki Mohamed Hussein kutokana na Shiza Kichuya kufanyiwa madhambi katika eneo la hatari.

Dakika ya 69 Ajib alipata nafasi ya kuifungia Simba goli la pili baada ya kupokea pasi safi toka kwa Mavugo lakini shuti lake lilinyakwa na mlinda mlango Agaba Oscar.

URA walionekana kujilinda zaidi huku wakifanya mashambulizi ya kushtukiza lakini Simba walikuwa imara zaidi kuokoa hatari zote zilizokuwa zikijitokeza.

Simba iliwatoa Mgosi, Mnyate, Kichuya na Ajib nafasi zao zikachukuliwa na Musa Ndusha,Hajji Ugando pamoja na Fredrick Blagnon.

Post a Comment

 
Top