BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
STRAIKA mpya wa Simba, Laudit Mavugo raia wa Burundi amewatoa hofu mashabiki wa Simba ambao wamekuwa na wasiwasi kwamba huenda atashindwa kuichezea timu hiyo baada ya kuwepo taarifa kuwa ana mkataba wa mwaka mmoja na timu yake ya zamani ya Vital'O. 

Mavugo ameiambia BOIPLUS kuwa hana mkataba na Vital'O ila kitu pekee anachowaomba viongozi wa Simba ni kwenda kumalizana haraka na timu yake iliyomkuza kisoka ya Solidarite ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kutoa ITC yake. 

Mavugo alisema kuwa siku 20 zilizobaki ni chache hivyo ni vyema kukamilisha jambo hilo haraka ili lisimzuie kukipiga Msimbazi msimu ujao wa Ligi Kuu Bara. 


"Kitu ninachowashauri viongozi wa Simba ni kumalizana haraka na timu yangu ya Solidarite hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kutoa ITC yangu na wameishikilia wao tangu irudishwe kutoka Rwanda, FIFA wanafahamu hilo na sheria ziko hivyo.

"Nafahamu kuna pesa Solidarite watahitaji ila sijajua ni kiasi gani, siku zimebaki chache wanapaswa kumalizana nao mapema ila mashabiki wa Simba wajue kwamba sina mkataba na Vital'O hayo ni maneno na mambo ya kunivuruga tu, mkataba ulipomalizika walitaka kuniongeza ila nilikataa kwa vile nadaiwa na Simba," alisema Mavugo.

Post a Comment

 
Top