BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda, Dar
Andrew Vicent mbele akiwa mazoezini, nyuma yake ni Juma Mahadhi na Simon Msuva

MLINZI wa kati wa mabingwa wa Tanzania Yanga, Andrew Vicent 'Dante' amewatoa hofu wapenzi na wanachama wa timu hiyo baada ya kuumia katika dakika za mwanzo za mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya Mo Bejaia hapo jana.

Akizungumza na BOIPLUS asubuhi ya leo Dante alisema anaendelea vizuri baada ya kupata matibabu jana huku akiamini anaweza kuanza mazoezi jumatatu hii kujiandaa na mchezo dhidi ya Azam.

"Nilipata maumivu makali nikaomba kutolewa, ila sasa sisikii maumivu kama jana, nitaanza mazoezi keshokutwa na Mungu akijalia nitakuwa tayari hata kwa mchezo wa Ngao ya Jamii na safari ya kuifuata Mazembe," alisema Dante.

Beki huyo wa zamani wa Mtibwa  Sugar mwenye nguvu na anayetumia mbinu katika ukabaji amekuwa hapati nafasi mara kwa mara katika kikosi cha kwanza lakini mwenyewe anaamini ipo siku mwalimu atamwamini.

"Niliumia sana roho kutoka jana, kiukweli nilipanga kuwaonyesha watu kile nilichonacho katika mechi kubwa kama ile. Lakini Mungu ndiye anajua, naamini siku nyingine nitapata nafasi ya kucheza na nitaonyesha uwezo ili kuisaidia timu yangu," alimaliza Dante. 

Dante alipata maumivu makali ya nyama za paja la mguu wa kulia baada ya kugeuka ghafla ili amrejeshee mpira kipa Deogratius Munishi 'Dida' na kupeleka kushindwa kuendelea na mchezo huo huku nafasi yake ikichukuliwa na Kelvin Yondan.

Yondan kulia akichuana na Morgan Betorangal wa Bejaia

Hata hivyo Yondan hatoruhusiwa kucheza mechi dhidi ya Mazembe baada ya jana kuzawadiwa kadi nyingine ya njano hivyo Yanga wanatakiwa kuhakikisha hali ya afya ya Dante inakaa vizuri mapema ili aweze kuwa 'fit' kwa ajili ya mchezo huo.

Post a Comment

 
Top