BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu, Dar
SHIRIKISHO la mpira wa miguu Tanzania TFF limeziambia klabu zinazoshiriki ligi kuu na zile za daraja la kwanza kwamba halitatoa leseni kwa wachezaji wao mpaka watakapokwenda kusajili mikataba ya wanandinga hao.

Kwa mujibu wa kanuni 68 (1,2,3 na 8) ya ligi kuu Tanzania bara inataka mikataba ya wachezaji kupitishwa na TFF ili kutoa leseni kwa wanandinga hao ambayo itakuwa ni kinga kwao katika majukumu yao ya kucheza mpira.

Kwa klabu zinazoshiriki ligi kuu watawalipia wachezaji wao kila mmoja shilingi elfu hamsini huku zile za ligi daraja la kwanza wakiwalipia elfu ishirini na tano kwa ajili ya kusajiliwa TFF.

Ofisa Habari wa TFF Alfred Lucas amewaambia waandishi kuwa mchezaji yoyote ambaye mkataba wake hautasajiliwa na shirikisho hilo hataruhusiwa kucheza mpaka atakaposajiliwa ili kuondokana na malalamiko yasio na msingi ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara.

Lucas alisema kuwa zitatolewa nakala tatu za usajili ambazo TFF itabaki na moja klabu nayo itachukua moja huku mchezaji pia akichukua yake moja kwa ajili ya ushaidi endapo kuna mtu ataenda kinyume na makubaliano.

"Kumekuwa na malalamiko mengi ya mikataba baina ya wachezaji na timu zao ndiyo maana wanatakiwa kuja kusajili mikataba yao hapo ili iwe rahisi kushughulikiwa" alisema Lucas.

Katika hatua nyingine Lucas alisema hakutakuwa na muda wa nyongeza kwa dirisha la usajili ambalo litafungwa wikiendi hii na kuzitaka klabu kufanya kila kitu kwa muda.

Post a Comment

 
Top