BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar 
MFUMO wa utumiaji wa tiketi za kilectroniki kwa mechi za ligi kuu ya Vodacom unatarajiwa kuanza kutumika siku chache zijazo baada ya mashine zake kukamilika kwa asilimia kubwa.

Mashine hizo zitafungwa kwenye mageti ya kuingilia uwanja wa Taifa ambapo mtu mmoja atahudumiwa kwa sekunde mbili huku dakika 180 zikitosha kuwahudumiwa mashabiki wote watakaohudhuria.

Katibu mkuu wa Wizara ya Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Elisante Ole Gabriel amemtaka Waziri Nape Nnauye kuhudhuria hafla ya kuzindua mashine hizo zitakazofanyika uwanjani hapo Septemba 4.

Katibu huyo alisema kuwa mashine hizo zimechelewa kuanza kutumika kwasababu zilikuwa zikifanyiwa majaribio ya kuweza kuwahudumia watu wengi kwa wakati mmoja ili kupunguza usumbufu kwa wapenzi wa soka.

"Kwa sasa mashine zimekamilika na tunamwalika Mheshimiwa Waziri kuja kufungua mashine hizi Septemba 4 hapa hapa uwanjani" alisema Ole Gabriel.

Kwa upande wake Waziri Nape alisema mfumo huo utasaidia Serikali kupata mapato kulinganisha na utaratibu wa vishina ambao ulikuwa ukiwanufaisha watu wachache ambao aliwataja kwa jina la 'Makomandoo'.

"Kwa mfumo huu sasa Serikali itaingiza mapato makubwa kupitia kodi itakayokatwa kwa kila tiketi itakayonunuliwa na wale wanaojiita Makomandoo watafute kazi nyingine ya kufanya" alisema Nape.

Post a Comment

 
Top