BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, Shinyanga
STAND United imeshindwa kutamba kwenye uwanja wake wa nyumbani baada ya kulazimishwa sare tasa na Toto Africans ya jijini Mwanza, mechi hiyo ya kirafiki imechezwa Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.

Hii ni mechi ya pili ya kirafiki kwa Stand United tangu waanze maandalizi yao ambapo juzi ilitoka sare ya bila kufungana na Alliance ya jijini Mwanza na kesho Jumapili Stand itarudiana na Alliance mjini Mwanza.

Mechi hiyo pia ilikuwa maalumu kwa ajili ya siku ya Stand United inayoazimishwa kila mwaka ambapo huwatambulisha wachezaji wao waliowasajili na wale wanaoendelea na mikataba yao kwa msimu ujao wa ligi kuu na wamesajili kikosi cha wachezaji 27.

Kocha wa Stand, Patrick Liewig ambaye aliwatumia nyota wake kibao amesema kuwa mechi hizo ni maalumu kuangalia mapungufu ya kikosi chake kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Bara wiki ijayo. 

Kwa upande wa kocha mkuu wa Toto, Rogacian Kaijage alisema kuwa timu yake inaendelea kuimarika na anagundua mapungufu kila mechi ya kirafiki anayocheza na kuyafanyia kazi.

"Ukiangalia kwa umakini Stand wapo vizuri lakini hata sisi pia kikosi chetu kipo imara zaidi ni makosa tu ya kiufundi ambayo nitayafanyia kazi, naamini tutafanya vizuri msimu ujao," alisema Kaijage

Toto watacheza mechi nyingine ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Black Eagle ya Burundi, mechi hiyo itachezwa Uwanja wa CCM Kirumba.

Post a Comment

 
Top