BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu ,Dar
KIUNGO wa Simba Jonas Mkude amefunguka kuwa alifuzu majaribio  katika klabu ya Mpumalanga inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini lakini kutokana suala la maslahi dili hilo limechelewa mpaka sasa.

Kiungo huyo alifanya majaribio  kwa muda wa wiki mbili ambapo alifanya vizuri na timu hiyo kuonekana kumuhitaji kiungo huyo fundi. Awali alikwenda kufanya majaribio katika timu ya Bidvest lakini hakufanikiwa.

Akizungumza  na BOIPLUS Mkude alisema  ni kweli alifanikiwa kufuzu  lakini  viongozi wa timu hiyo  walishindwana  bei na Simba ambao ndiyo waajiri wake ndiyo maana dili likakwama. 

"Walikuwa wanahitaji huduma yangu lakini nikiangalia masilahi ni madogo nikaamua kuwaachia wamalizane na uongozi wa Simba pamoja na Meneja wangu," alisema Mkude.

Kiungo huyo bado ana matumaini ipo siku ataagana na Simba na kutimka zake nje ya nchi huku akisema kuna timu ipo Afrika Kusini bado inataka kumsajili  ila kinachomkwamisha ni  mkataba wake na Simba .

Aidha Nahodha  huyo msaidizi wa Simba alisema matokeo ya magoli 4-0 waliyoyapata dhidi ya AFC Leopards ni mazuri na yameongeza chachu kwa kikosi cha Wekundu hao  kufanya vizuri katika ligi itakayoanza wiki mbili zijazo.

Simba imesherehekea vyema miaka 80 jana kwa kutambulisha wachezaji wake, jezi zitakazotumika msimu huu pamoja na benchi zima la ufundi la klabu hiyo katika sherehe zilizohudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali wakiwemo Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda na Naibu Waziri wa afya na Ustawi wa Jamii Hamisi Kigwangala.

Post a Comment

 
Top