BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu
TIMU ya Yanga imewasili salama mjini Lumbumbashi nchini DR Congo tayari kwa mchezo wa kukamilisha ratiba wa kombe la shirikisho barani Afrika dhidi ya TP Mazembe utakaopigwa siku ya Jumanne.

Yanga iliondoka asubuhi ya leo kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways) ikiwa na wachezaji 19 na viongozi tisa wakiwemo mwakilishi wa TFF na kaimu katibu mkuu wa klabu hiyo Baraka Deusdedith.


Akiongea na BOIPLUS Meneja  wa Yanga Hafidh Saleh alisema wamefikia salama mjini Lubumbashi na wamepata mapokezi mazuri kutoka kwa Watanzania wanaoishi nchini humo.

"Wachezaji wote wapo katika hali nzuri, na tunashukuru watanzania wanaoishi hapa Lubumbashi wanatupa 'sapoti' kubwa japokuwa mechi yetu ni ya kukamilisha ratiba tu," alisema Hafidh.


Kwa upande wake mshambuliaji raia wa Burundi Amissi Tabwe alisema hata kama wameshatolewa katika michuano hiyo lakini watajitahidi kuibuka na ushindi kwa ajili ya heshima.

"Tumejifunza mambo mengi katika michuano hii na mwakani tukirudi tutakuwa bora zaidi, chamsingi ni kushinda mechi hii ili kukamilisha ratiba kwa heshima," alisema Tambwe.


Yanga tayari imeshaondolewa katika michuano hiyo ikiwa  na alama tano baada ya kushuka dimbani mara tano na ndio wanashika mkia kwenye kundi A lililokuwa na timu za Mazembe, MO Bejaia, na Medeama.

Post a Comment

 
Top