BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma,Dar
TIMU ya Yanga imefufua matumaini ya kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Mo Bejaia mchezo uliopigwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Dakika ya pili tu mshambuliaji Amissi Tambwe aliipatia Yanga goli la kuongoza kufutia mpira wa adhabu uliopigwa na Juma Abdul kutokana na mabeki wa Bejaia kumchezea rafu Simon Msuva nje kidogo ya eneo la hatari.

Baada ya goli Bejaia waliamka na kuongeza kasi ya mashambulizi ambapo dakika ya 16 almanusura wasawazishe lakini umahiri wa golikipa Deogratius Munishi 'Dida' ulisaidia kuondoa hatari.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa timu zote kushambuliana kwa zamu ambapo dakika ya 49 Mohamed Yacine Athumani alikosa goli la wazi baada ya kubaki na kipa na shuti lake likawa mboga kwa Dida.

Dakika kumi baadae Msuva alitengenezewa nafasi ya kufunga na Obrey Chirwa lakini umakini ukawa mdogo. Dakika ya 70 Chirwa nae alikosa goli baada ya kuunganisha krosi ya Msuva.

Yanga iliwatoa Vicent Andrew, Juma na Deus Kaseke nafasi zikachukuliwa na Kelvin Yondani, Saidi Makapu pamoja na Juma Mahadhi ambaye alionesha kiwango safi.

Yanga imesaliwa na mchezo mmoja dhidi ya vinara TP Mazembe utakaochezwa kati ya Agosti 23 na 24 mjini Lubumbashi katika mechi ambayo mabingwa hao watatakiwa kushinda na kuwaombea Bejaia na Medeama watoke sare ili kuweza kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali na hiyo kama Mazembe wataifunga Medeama kesho.

Yanga inaendelea kuburuza mkia katika kundi A licha ya kupata ushindi huo ambao sasa wamefikisha alama nne.

Post a Comment

 
Top