BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
TIMU ya Yanga imeshindwa kuionyesha ubabe Mtibwa Sugar baada ya timu hizo kutoka sare ya bila kufungana katika mchezo wa kujipima nguvu uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo ulianza taratibu huku timu zote zikishambuliana kwa zamu lakini Yanga ndiyo walifika zaidi langoni mwa Mtibwa ingawa jitihada zao hazikuzaa matunda.

Mechi ilipendeza zaidi eneo la kati ya kiwanja ambapo Saidi Makapu na Thaban Kamusoko waking'aa upande wa Yanga huku Ibrahim Jeba pamoja na Ally Makarani wakitisha kwa Wakata miwa.

Dakika ya 27 Mshambuliaji Matheo Anthony alikosa goli la wazi baada ya Obrey Chirwa kuichambua safu ya ulinzi ya Mtibwa na kumtengea mchezaji huyo akibaki na mlinda mlango Abdallah Makangana na kupiga shuti lililopaa juu ya lango.

Wachezaji Chirwa, Said Makapu na Mwinyi Haji walikuwa katika ubora mkubwa na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa timu hiyo kila walipogusa mpira.

Yanga ilimpumzisha Matheo nafasi ikachukuliwa na kinda Yusuph Mhilu huku Mtibwa wakiwatoa Mohamed Issa, Jeba na Rashidi Mandawa wakawaingiza Shaban Nditi, Jaffari Salum pamoja na Vicent Barnabas.

Post a Comment

 
Top