BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
KLABU ya Azam FC imeendelea kusisitiza kutumia uwanja wake wa Azam Complex kwenye mechi zake zote za nyumbani katika ligi ya Vodacom Tanzania bara inayoendelea hata kwenye michezo inayohusisha Simba na Yanga.

Kwa wiki kadhaa sasa kumekuwa na mijadala  mbali mbali kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uhalali wa uwanja huo kutumika hasa katika mechi zinazozihusisha timu za Simba na Yanga kutokana na uwezo wake wa kuingiza mashabiki.

Uwanja wa Azam Complex unaweza kuingiza mashabiki 7000 pekee huku klabu hizo kongwe nchini zikiwa na mashabiki wengi kuzidi uwezo wa dimba hilo hali inayoweza kuhatarisha amani.

Mkurugenzi Mtendaji wa klabu hiyo Saad Kawemba alisema msimamo wa klabu yake ni kutumia uwanja wao wa nyumbani kwakua ndiyo sababu ya kujengwa kwa dimba hilo.


Kuhusu mapato kuwa chini endapo watatumia uwanja huo katika mechi zinazoshirikisha Simba na Yanga Kawemba alisema "Mapato ya mlangoni ni kwa ajili ya timu mwenyeji, sisi kama Azam FC tupo tayari kupata hasara lakini mechi zetu zichezwe Azam Complex.

"Arsenal FC walikuwa wanatumia uwanja mdogo wa Highbury baada ya kuona wanakosa mapato wakajenga mkubwa wa Emirates kwahiyo hata sisi tukiona tunahitaji mapato zaidi tutaongeza dimba letu," alisema Kawemba.

Kawemba alisema pia endapo Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF litawagomea kucheza mechi za Simba na Yanga kwenye uwanja wao basi wasiseme kuwa Azam ni mwenyeji kwenye michezo hiyo.

"Azam haiwezi kuwa timu mwenyeji kwenye uwanja wa Taifa au Uhuru bali ni Azam Complex pekee ndiyo wana mamlaka yakuwa wenyeji kwenye mchezo wowote kwahiyo wasiseme kama sisi tuko nyumbani," alimalizia Kawemba.

Post a Comment

 
Top