BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu,Dar
NAHODHA wa timu ya Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amekubali kuwa itakuwa ngumu kuendelea kuwa tegemeo kikosini kutokana na majeruhi yanayo muandama huku kukiwa na mabeki wazuri waliosajiliwa na mabingwa hao.

Cannavaro alitengeneza uelewano mzuri na beki Kelvin Yondani kwa misimu zaidi ya mitatu na kuwa miongoni mwa safu bora za ulinzi kwenye klabu ya Yanga na timu ya Taifa lakini majeraha ya mara kwa mara yamekuwa yakipunguza ufanisi wake dimbani.

Nahodha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ameiambia BOIPLUS kuwa uwepo wa mabeki vijana wenye uwezo mkubwa ndani ya kikosi  cha mabingwa hao umefanya kupungua kwa umuhimu wake ndani ya Yanga.

"Majeraha yamenisumbua sana halafu pia kuna mabeki wapya ambao nao wanatekeleza majukumu vizuri pindi wawapo uwanjani na kuisaidia timu kupata matokeo mazuri,"   alisema Cannavaro.

Cannavaro ambaye ana umri wa miaka 34 sasa anapigania namba na mabeki Vicent Bossou, Yondani na Vicent Andrew 'Dante' ambaye msimu uliopita alikuwa akichezea Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro.

Beki huyo kisiki alianza kuaminiwa na kupata namba kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga  msimu wa 2007/08 na alikabidhiwa kitambaa cha unahodha msimu wa 2013/14, baada ya kustaafu kwa kiongozi wa awali, Shadrack Nsajigwa.

Yanga inatarajiwa kushuka dimbani kesho kumenya na Majimaji katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam mchezo ambao unatarajiwa kuwa mgumu kutokana na matokeo yaliyotangulia.

Post a Comment

 
Top