BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu
KAMATI ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji iimeahirisha kikao chake kilichokuwa kikae kesho Jumapili Septemba 4, kutoa hukumu ya shauri la mchezaji Hassan Ramadhan Kessy anayedaiwa na Klabu ya Simba kuvunja mkataba kwa kuanza kufanya mazoezi na klabu ya Yanga sambamba na kusajili katika timu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Jangwani kabla ya mkataba wake kufika mwisho Juni 15, 2016.

Simba imelalamika mbele ya kamati hiyo ya kuwa, mchezaji Kessy alivunja taratibu hizo akiwa ndani ya mkataba wa klabu hiyo. Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati hiyo, shauri hilo litasikilizwa baadaye mwezi huu katika tarehe itakayopangwa.

Sababu za kuahirisha kikao hicho ni kutotimia kwa akidi ya wajumbe wa kamati nzima. Akidi ni lazima wajumbe zaidi ya watatu wathibitishe kushiriki.

Ilikuwa isikilizwe kesho baada ya kushindikana kusikilizwa kwa shauri jingine linalohusu Klabu ya Simba ikiilalamikia Yanga kuingia mkataba na mchezaji Kessy wakati bado ana mkataba na Wekundu hao.

Shauri la Simba dhidi ya Yanga lilishindika kusikilizwa kwa sababu vijana hao wa jangwani hawakutokea mbele ya kamati  hivyo kuandikiwa barua  kukumbushwa kuhudhuria kwenye kesi hiyo Jumapili ijayo kabla ya kutolewa uamuzi.

Kama hawakutokea tena, shauri hilo litasikilizwa upande mmoja na kutolewa uamuzi upande mmoja. Kadhalika mashauri mengine yatakayosikilizwa hapo baadaye ni pamoja na yale ambayo wahusika walipewa nafasi ya kuyamaliza nje ya kamati lakini wakashindwa.

Post a Comment

 
Top