BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma,Dar
BENKI ya Diamond Trust Bank DTB imesaini mkataba na Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) wenye thamani ya sh 250 milioni kwa ajili ya kudhamini ligi kuu ya Vodacom kwa mwaka mmoja.

Akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini uliofanyika kwenye Hotel ya Serena Mkuu wa kitengo cha Fedha wa Benki hiyo Joseph Mabusi alisema udhamini huo utasaidia maendeleo ya soka nchini kwa kuziwezesha timu shiriki kujiandaa vya kutosha ili kuwa na ligi bora yenye ushindani wa kweli.

"Tunafurahi na kujivunia kuwa sehemu ya soka tunawaahidi wadau wa soka kuendelea kuwa pamoja nao kwa muda mwingi zaidi licha ya kusaini mwaka mmoja,"alisema Mabusi.Kwa upande wake Rais wa TFF Jamal Malinzi ameishukuru benki hiyo kujitokeza kudhamini ligi huku akitanabaisha kuwa udhamini huo umefika muda muafaka kutokana na Shirikisho kuandamwa na mambo mengi yanayohitaji fedha.

"Ninawashukuru DTB kwa kujitokeza kudhamini, na pia nichukue nafasi hii kuyakaribisha makampuni mengine kuendelea kujitokeza ili tuweze kuwa ligi bora," alisema Malinzi.

Nae Mwenyekiti wa bodi ya ligi Hamadi Yahaya ameitoa hofu Benki hiyo kuwa pesa zilizotolewa zitaenda kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa huku wakijiandaa kukaa na timu shiriki ili kuangalia jinsi ya kuzigawa.

Wakati huo huo Mwakilishi wa klabu ambaye ni Mwenyekiti wa African Lyon Rahim Zamunda alisema kuwa ili taifa liweze kufika mbali katika medani ya soka lazima uwekezaji mkubwa uendelee kufanywa na makampuni mbali mbali kwakua mpira ni ajira kwa sasa.

Post a Comment

 
Top