BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
BAADA ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 toka kwa Ndanda FC wikiendi iliyopita kikosi cha Azam FC kimeanza mazoezi leo hii kwa ajili ya kuwavutia kasi Maafande wa Ruvu Shooting utakaopigwa uwanja wa Azam Complex.

Afisa Habari wa 'Wana lambalamba' hao Jaffar Iddi Maganga alisema baada ya mchezo dhidi ya Ndanda wachezaji walipewa mapumziko mafupi ya siku tatu kabla ya leo kuanza mazoezi kwa ajili ya mchezo dhidi ya Maafande hao wa Mlandizi mkoani Pwani.

"Kikosi kimeanza mazoezi leo baada ya mapumziko ya muda mfupi chini ya kocha wetu Zeben Hernandez kikubwa ni kutafuta ushindi kwenye mchezo wetu wa wiki ijayo," alisema Jaffar.

Aidha Jaffar alisema bado hawajakata tamaa ya kuchukua ubingwa msimu huu kwakua bado ligi ni mbichi huku wakiwa wamebakiwa na michezo mingi mkononi licha ya kupata matokeo mabovu katika siku za hivi karibuni.

"Bado tupo kwenye mbio za ubingwa, ligi bado mbichi sana hatujakatishwa tamaa na matokeo haya, tunaendelea kujipanga ili kuhakikisha tunafanya vizuri," alisema Jaffar.

Msemaji huyo alisema moja ya sababu iliyopelekea kutofanya vizuri kwenye michezo yao ya karibuni ni majeruhi yanayowaandama wachezaji wao hasa safu ya ulinzi.

"Kwenye michezo yetu miwili dhidi ya Simba na Ndanda tuliwakosa mabeki wetu Pascal Wawa, Erasto Nyoni na Agrey Moris kitu ambacho kimetugharimu sana," alimaliza Jaffar.

Post a Comment

 
Top