BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
MIAMBA ya soka nchini Simba na Yanga inatarajia kukutana kesho kutwa  Jumamosi Oktoba mosi kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mtanange ambao unatikisa nchini nzima. Kuelekea mchezo huo kumekuwa na tambo mbali mbali kutoka kwa upande zote mbili lakini dakika 90 za mtanange huo zitaamua nani ataibuka mbabe.

Simba ndiyo kinara wa ligi hiyo akiwa na alama 16 huku Yanga wakiwa nafasi ya tatu baada ya kujikusanyia pointi 10 wakiwa na mchezo mmoja mkononi. Kwa kawaida mchezo huo unakuwa na presha kubwa kuanzia kwa wachezaji, viongozi hadi mashabiki. Mara kadhaa makocha wametimuliwa kazi kutokana na matokeo ya mechi hizi hata kama siyo za ligi.

Wafuatao ni wachezaji 11 (kikosi kizima) ambao 'Derby' hii ya Jumamosi itakuwa ni ya kwanza kwao lakini bado wana uwezo wa kufanya maajabu katika mchezo huo.

Straika wa Simba Laudit Mavugo
 
1. LAUDIT MAVUGO
Mshambuliaji huyo raia wa Burundi aliyekuwa akikipiga katika klabu ya Vital'O ya nchini humo amegeuka kuwa kipenzi cha Wanasimba na kuwa miongoni mwa nyota wanaotegemewa kufanya vizuri katika mchezo huo. 

Mpaka sasa mshambuliaji huyo amaeshafunga mabao matatu katika michezo sita aliyoshuka dimbani japokuwa kiwango chake katika mechi mbili za mwisho hakijawaridhisha sana wanasimba hao. Hali hii haiwezi kumzuia kuidhuru Yanga kama atapata nafasi.

2. OBREY CHIRWA
Huyu ni raia wa Zimbabwe ambaye ndiye anashikilia rekodi ya kusajiliwa kwa dau kubwa katika ligi ya Vodacom, bado hajafanya vizuri sana baada ya kutofunga bao lolote tangu ajiunge na Yanga mwezi Julai. 

Mashabiki wengi wa soka hawampi nafasi ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo lakini Chirwa ana kipaji kikubwa, anaweza akaibuka shujaa na kuwanyamazisha wote wanaomkosoa. Simba wanapaswa kuwa makini nae asije akaibuka kwenye mechi hiyo.
 Obrey Chirwa

3. FREDRICK BLAGNON
Mshambuliaji huyo raia Ivory Coast ana uwezo wa kupiga mipira ya vichwa kutokana na urefu wake, naye atakuwa anacheza mechi hiyo kwa mara ya kwanza. Mabeki wa Yanga watapaswa kuwa makini nae kwakua Simba wana wachezaji wazuri wa kupiga mipira ya krosi hasa Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr'.

4. VICENT ANDREW 'DANTE'
Beki wa zamani wa Mtibwa Sugar ambaye amekuwa kwenye ubora mkubwa tangu ajiunge na mabingwa hao msimu huu. Licha ya kuwa na umbo fupi lakini beki huyo ni hodari kwa mipira ya juu kitu kinachompa sifa ya kucheza mbele ya mabeki wazoefu wa Yanga Kelvin Yondani na Nadir Haroub.

Ni mlinzi anayetumia sana akili, washambuliaji wa Simba wakiingia kwa imani kwamba ni mgeni  wa mechi ya watani basi wanaweza kutoka patupu.
Andrew Vicent 'Dante' kulia alipokuwa akiitumikia Mtibwa Sugar. Hapa alikuwa akimdhibidhi Donald Ngoma ambaye sasa anakipiganae kwa Wanajangwani.

5. SHIZA KICHUYA.
Kichuya mpaka sasa ni miongoni mwa wachezaji wanaongoza kwa ufungaji baada ya kutupia nyavuni mabao manne katika ligi. Winga huyo wa zamani Mtibwa Sugar amekuwa msaada mkubwa kwa Simba kutokana na kasi yake uwanjani kitu ambacho mabeki wa Yanga wanapaswa kumchunga sana kwenye mchezo huo.

6. JUMA MAHADHI
Mahadhi ni kijana ambaye ameingia moja kwa moja kwenye kikosi cha Kocha Hans Pluijm kutokana na uwezo wake. Winga huyo wa zamani wa Coastal Union katika mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe uliopigwa hapa Dar alionesha uwezo mkubwa kwa kuwasumbua mabeki kutoka upande wa kushoto na kupiga krosi zenye madhara.

Ugeni wake katika mchezo huu hauwezi kumzuia kinda huyo kuwapa wakati mgumu walinzi wa Simba. Hapa ni lazima wawe makini ili kuepuka madhara yake.
Juma Mahadhi akishangilia bao mbele ya kocha wake Hans Pluijm

7. MUZAMIRU YASSIN
Kiungo mkabaji mwenye uwezo mkubwa wa kupandisha timu, amejihakikishia namba katika kikosi cha Kocha Joseph Omog baada ya kutengeneza ushirikiano mzuri na nahodha Jonas Mkude ambao umeifanya safu ya kiungo kuwa imara zaidi. 

Msimu uliopita Muzamiru alikuwa akiwatumikia wakata miwa wa Mtibwa Sugar na kwamba hii itakuwa mechi yake ya kwanza ya watani wa jadi.

8. BENNO KAKOLONYA.
Mlinda mlango huyu wa zamani wa Tanzania Prisons ambaye alikuwa katika kiwango bora amekuwa hapati nafasi katika kikosi cha Yanga. Tangu ajiunge na mabingwa hao bado hajacheza mechi yoyote mbele ya Dida na Barthez lakini bado ni kipa mzuri na endapo atapewa nafasi katika mchezo huo anaweza kufanya vizuri na kuushangaza umma.

9. JAMAL MNYATE
Hakuna ambaye alitarajia winga huyu wa zamani wa timu ya Mwadui FC angeingia moja kwa moja kikosi cha kwanza cha Simba. Lakini uwezo mkubwa aliouonyesha umemuweka katika orodha ya wachezaji muhimu kikosini huku tayari akiwa ameshafunga mabao mawili. 

Katika mchezo dhidi ya Majimaji wikiendi iliyopita winga huyo alikuwa kwenye ubora mkubwa na hii inaweza kumpa morali kuelekea Kariakoo Derby.

Beki wa kulia wa Simba Janvier Bukungu

10. JANVIER BUKUNGU.
Bukungu aliwahi kuchezea TP Mazembe kwa mafanikio na sasa amekuwa akiaminiwa kucheza beki wa kulia katika kikosi cha Simba. Bukungu hana kasi uwanjani lakini anafanya kazi yake kwa umakini mkubwa ni nadra kumuona akifanya makosa uwanjani. 

Hana mambo mengi na hajichoshi, anatimiza wajibu wake tu kwanza, washambuliaji wa Yanga wasitarajie kumfanya uchochoro kwavile ni nadra kumuona akipanda mbele.

11. MOHAMED IBRAHIM
Bado hajapata nafasi kubwa ya kucheza ndani ya kikosi cha kwanza cha Simba lakini kwenye mchezo dhidi ya Majimaji kiungo huyo aliingia kipindi cha pili na kufanya kazi nzuri.

Hii inaweza kumshawishi kocha Omog kumpa nafasi katika mchezo huo wa Jumamosi na akaisaidia timu.

Post a Comment

 
Top