BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu, Dar
PAMBANO la watani wa jadi Simba na Yanga limekuwa likivuta hisia za watu wengi sana toka ndani na nje ya nchi tangu miamba hiyo ilivyoanzishwa kutokana ushindani uliopo baina ya timu hizo.

Muigizaji nyota wa Bongo Movies Miriam Jolwa  maarufu kama 'Jini Kabula' ambaye ni shabiki wa damu wa timu ya Yanga ametamba kikosi chake kitaibuka na ushindi kwenye mchezo wao utakaopigwa Oktoba mosi kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kutokana na uimara wa kikosi chao ukilinganisha na wapinzani wao Simba.

 Jini Kabula aliyetamba sana katika tamthiliya ya 'Jumba la dhahabu' iliyoandaliwa na muongozaji Tuesday Kihangala na kurushwa na Shirika la utangazaji la Taifa TBC 1 alisema kwa sasa hakuna timu ya kuisumbua Yanga licha ya kukubali kichapo toka kwa Stand United wikiendi iliyopita.


Kabula ameiambia BOIPLUS kuwa anakiamini kikosi chake kwakua kipo kwenye ubora mkubwa huku wakiwa mabingwa watetezi kwahiyo amewahakikishia Watani wao kuwa kichapo kipo pale pale.

“Sisi mashabiki wa Yanga hatuna wasi wasi na timu yetu tunategemea kuibuka na ushindi mkubwa kama msimu uliopita na jeuri hiyo tunayo kwakua tuna kikosi imara kuliko Simba," alisema Kabula ambaye ni mhudhuriaji mzuri wa mechi za Yanga.

Aidha muigizaji huyo amewataja washambuliaji Donald Ngoma na Amissi Tambwe kuwa ndiyo watu watakao peleka kilio kwa Wana Simba Jumamosi pale uwanja wa Taifa.

"Sijaona beki wa kuwazuia Ngoma na Tambwe wasifunge kwenye kikosi cha Simba, nawaomba watani wakae mkao wa kuumizwa wikiendi ijayo," alimaliza Kabula.

Post a Comment

 
Top