BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Dar
MAAFANDE wa JKT Ruvu wamewasili salama jijini Mwanza leo asubuhi tayari kwa mtanange dhidi ya Mbao FC mchezo utakaofanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba keshokutwa Jumapili Oktoba 2.

Maafande hao chini ya Kocha Malale Hamsini wapo katika hali nzuri ya kiafya huku wakiwa na morali kubwa ya ushindi hasa baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City kwenye uwanja wa Mabatini wikiendi iliyopita.

Afisa Habari wa Maafande hao Afisa Mteule daraja la pili Constantine Masanja ameiambia BOIPLUS kuwa wamejipanga kuhakikisha wanaondoka na alama zote tatu ugenini toka kwa 'Wapiga randa' hao wa jiji la Mwanza kutokana na maandalizi mazuri waliyofanya.

"Tumewasili salama jijini hapa asubuhi ya leo timu iko vizuri, benchi la ufundi na watu wote tuliopo huku tunasubiri tu muda ufike tuingie uwanjani kucheza mchezo wetu" alisema Masanja.

Aidha Masanja alisema katika mchezo huo watawakosa nyota wao watatu ambao ni Michael Aidan, Nurdin Mohamed pamoja na Hassan Dilunga ambao hawakusafiri na timu kutokana na majeruhi.

"Tutawakosa nyota wetu watatu lakini haituzuii kuibuka na ushindi kwenye mchezo wetu wa Jumapili kwakua tuna kikosi kipana," alisema Masanja.

Post a Comment

 
Top