BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Dar
KUELEKEA mchezo wao dhidi ya Maafande wenzao wa Ruvu Shooting (Mlandizi Derby) timu ya JKT Ruvu imejipanga kuwapigisha kwata Wanajeshi wenzao Jumamosi Septemba 10.

Mchezo huo unatarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi wa soka wa mkoa wa Pwani kutokana na uimara wa vikosi vyote katika michezo ya ligi iliyoshuka dimbani.

Mtanange ambao utakaofanyika kwenye uwanja wa Mabatini unakuwa wa kwanza baada ya mwaka mmoja kutokana na Ruvu Shooting kushuka daraja msimu wa 2015/16.

Afisa Habari wa Ruvu Constantine Masanja ameiambia BOIPLUS kuwa kikosi chao kinaendelea kujifua kwenye uwanja wa JKT Mbweni ili kuwapigisha kwata 'Wajeda' wenzao wa Shooting.

"Kikosi chetu kiko vizuri kinaendelea na kambi yake na jambo la kushukuru ni kuwa hatuna majeruhi hivyo tuko tayari kwa ushindi,"alisema Masanja.

Wachezaji Hassan Dilunga na Michael Aidan waliwahi kuchezea Shooting huku Abraham Mussa, Damas Makwaya, Issa Kanduru pamoja na Jabir Aziz Stima nao kwa nyakati tofauti waliitumikia Ruvu.

Kocha Mkuu wa Shooting Seleman Mtungwe 'Garincha' aliwahi kuwa nyota wa Ruvu miaka 80 na timu za Majeshi kitu ambacho kitachagiza ubora wa mchezo huo ambao wote wanatumia uwanja wa Mabatini kama uwanja wa nyumbani.

Post a Comment

 
Top