BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu ,Dar
BAADA ya kuibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Mbao FC wikiendi iliyopita timu ya Mwadui FC imejipanga kutoa kichapo kingine ugenini kesho itakapocheza na Kagera Sugar kwenye uwanja wa Kaitaba.

Kocha wa timu hiyo Jamhuri Kihwelo 'Julio' amejinasibu kuondoka na alama zote tatu kutokana na aina ya wachezaji aliokuwa nao ambao wamejipanga kufanya vema msimu huu.

Akizungumza na BOIPLUS Julio alisema  wamejipanga kushinda kila mchezo ulio mbele yao na kutoa ushindani wa kweli japokuwa katika mpira wa miguu lolote linaweza kutokea.

"Kikosi chetu kipo vizuri na wachezaji wote wana morali ya  kushinda ili kupata alama tatu ambazo zitazidi kutuweka kwenye mazingira mazuri" alisema Julio 

Kwa upande wake Kocha wa Kagera Sugar  Mecky Mexime alisema anatarajia  mechi itakuwa ngumu kwa timu zote ila wamejipanga kushinda katika uwanja wao wa nyumbani. 

Kocha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar alisema ligi ya msimu huu ina ushindani mkubwa kutokana na timu nyingi kujiandaa vizuri huku zikifanya usajili makini.

Mchezo huo utakuwa ni wa kwanza wa ligi kwenye uwanja wa Kaitaba tangu kukamilika kwa marekebisho yake yaliyochukua miaka miwili.

Michezo mingine ya ligi hiyo itakuwa ni Mbao FC dhidi ya Mbeya City, Majimaji itakayopepetana na Mtibwa Sugar huku JKT Ruvu wakiikaribisha African Lyon.

Post a Comment

 
Top