BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
KOCHA Kali Ongala anatarajia kusafiri kesho kuelekea Songea kwa ajili ya kukinoa kikosi cha Majimaji 'Wanalizombe' baada ya kumalizana na uongozi wa timu hiyo.

Ongala ambaye alikinoa kikosi hicho msimu uliopita alishindwa kuongeza mkataba na kujiweka pembeni hali iliyopelekea kuyumba kwa Wanalizombe hao na kujikuta wakipoteza michezo yote sita ya ligi iliyoshuka dimbani mpaka sasa.

Ongala amezungumza na kituo cha Radio cha EFM kwenye kipindi cha E Sports kuwa tayari ameshamalizana na mabosi hao na kila kitu kipo sawa na kesho atasafiri kuelekea Songea tayari kukinoa kikosi hicho.

"Tushamalizana na uongozi na kesho naenda Songea kwa ajili ya kuendelea kuifundisha Majimaji kama ilivyokuwa msimu uliopita,"alisema Ongala.

Aidha mchezaji huyo wa zamani wa timu za Yanga na Azam aliwataka mabosi wake wawalipe stahiki zao Wachezaji wote kabla ya kusaini kandarasi mpya ili wawe na moyo wa kujituma kwakua mpira kwa sasa ni ajira.

" Hauwezi kupata matokeo mazuri kama wachezaji hawajalipwa mishahara yao, nimeongea na uongozi kuhusu hilo na kila kitu kimeenda sawa,"alisema Ongala.

Ongala alisema pia ataendelea kufanya kazi na benchi la ufundi lililokuwa chini ya kocha Peter Mhina kwa ajili ya kuhakikisha wanarudisha furaha kwa wakazi wa mkoa wa Ruvuma.

Post a Comment

 
Top