BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda, Dar
KIKOSI cha Kinondoni Municipal Council 'KMC' kimeitandika Friends Rangers mabao 3-0 katika mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye dimba la Kinesi jijini Dar es Salaam jioni ya leo.

Timu hizo ambazo zinajiandaa na michuano ya ligi daraja la kwanza 'FDL' ziliuanza mchezo huo kwa kushambuliana kwa zamu lakini winga kinda wa KMC, Cliff Buyoya ndiye aliyefungua kitabu cha mabao kwa kuwaua mabosi zake hao wa zamani katika dakika ya 18 akimalizia kazi nzuri ya kiungo Joseph John.

KMC inayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni walipata bao la pili dakika ya 60 baada ya Joseph kufanya tena kazi ya ziada kabla hajamtengea Rashid Roshwa ambaye hakufanya ajizi na kuwanyanyua mashabiki wa timu hiyo.

Dakika 10 kabla pambano hilo halijamalizika, kona iliyochongwa na Iddy Suleman ilijaa moja kwa moja nyavuni na kuiandika KMC bao la tatu na la mwisho katika mchezo huo ambao umewasaidia makocha wa timu zote mbili kujua ubora na mapungufu ya vikosi vyao kabla ligi haijaanza.

Post a Comment

 
Top