BOIPLUS SPORTS BLOG

Uyo,Nigeria
TIMU ya Taifa ya Nigeria imedondosha hadi jasho la mwisho Taifa Stars bao 1-0 katika mchezo wa kufuzu mataifa Afrika uliopigwa kwenye uwanja wa Akwa Ibom International Stadium.

Katika mchezo huo wenyeji walianza kwa kasi dakika ishirini za mwanzo huku Stars wakicheza kwa umakini mkubwa hasa katika safu ya ulinzi iliyokuwa chini ya David Mwantika pamoja na Andrew Vicent 'Dante'.

Mlinda mlango Aishi Manula alikuwa kwenye ubora mkubwa baada ya kupangua michomo mingi ya washambuliaji wa 'Super Eagles' waliokuwa wakiongozwa Victor Moses pamoja na Odian Ighalo anayechezea Watford na Ahmed Mussa wa Leicester city zote za Uingereza.

Kipindi cha pili Manula aliendelea kuwabania wenyeji baada ya kufuta kila hatari iliyokuwa ikielekea nyavuni huku walinzi wa Stars wakifanya kazi ya ziada kumpunguzia idadi ya majaribu.

Dakika ya 66 Stars walifanya shambulio kali langoni mwa Nigeria baada ya kupiga gonga nyingi lakini shuti lililopigwa na Simon Msuva kutokana na pasi ya Faridi Mussa lilidakwa vizuri na mlinda mlango.

Dakika ya 77 mshambuliaji anayeichezea Manchester City ya Uingereza, Kerechi Iheanacho aliwapatia wenyeji goli la ushindi baada ya kupiga shuti kali akiwa nje ya 18 baada ya kupokea mpira uliotokana na  kona fupi.

Mchezo huo ulikuwa ni wa kukamilisha ratiba tu kwavile tayari Misri ilishafuzu katika kundi hilo.

Post a Comment

 
Top