BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu,Dar
BAADA ya kupokea vichapo mfululizo, kocha Mkuu wa Majimaji Peter Mhuna amepanga kufanya usajili mkubwa kwenye dirisha dogo la mwezi Novemba ili kujinusuru na janga la kushuka daraja.

Mhuna aliichukua timu hiyo muda mfupi kabla ya kuanza kwa ligi na hivyo kushindwa kufanya maandalizi ya kutosha kitu kinachopelekea kupokea vipigo hivyo baada ya kuchukua nafasi ya kocha Kali Ongala alioachana na 'Wanalizombe' mwezi Julai. 

Majimaji  wamepoteza mechi zao zote walizoshuka dimbani tangu kuanza kwa ligi anbazo ni dhidi ya Tanzania Prisons, Azam FC,  Mtibwa Sugar, kabla ya kichapo cha mabao 3-0 toka kwa mabingwa watetezi Yanga.

Mhuna ameiambia BOIPLUS kuwa anapaswa kufanya usajili mkubwa kwenye kikosi hicho kutokana na wachezaji wengi kushindwa kukidhi viwango vya kuitumikia timu hiyo  ili kuepuka janga la kushuka daraja.

“Nimezungumza na viongozi wangu tunasubiri dirisha dogo ili tuweze kusajili vijana wa kutuongezea nguvu katika timu yetu ambayo imekuwa na mwenendo mbovu, lengo mi kuangalia jinsi ya kuweza kuinusuru," alisema Mhuna.

BOIPLUS inafahamu kuwa wachezaji wa klabu hiyo hawajalipwa stahiki zao kwa muda mrefu kitu ambacho kinashusha morali ya kupambana kwa wanandinga hao.

Wikiendi ijayo Majimaji watakuwa nyumbani kuwakaribisha Ndanda FC mchezo ambao watatakiwa kushinda ili kujiweka kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa ligi.

Post a Comment

 
Top