BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
MKUU wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa michuano ya Wushu Tanzania itakayofanyika Septemba 17 na 18 kwenye uwanja wa Taifa kuanzia saa 4 asubuhi.

Mchezo wa Wushu ambao asili yake ni nchini China unajumuisha Karate, Kung Fu, Judo na aina zote za michezo yote ya mapigano kitu ambacho kitakuwa ni kivutio kikubwa kwa watakaohudhuria.

Mashindano hayo yatahusisha washiriki mbali mbali toka mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani,Morogoro, Lindi, Mtwara, Pemba pamoja na Mbeya.

Rais wa chama cha Wushu Tanzania Mwalami Mitete alisema washindi wa mashindano hayo watapata medali, fedha taslimu, vikombe, Simu za mkononi pamoja na vyeti vya utambulisho ambavyo vitawawezesha kushiriki mashindano mbali mbali ndani na nje ya nchi.

Mitete alisema kuwa kumekuwa na dhana potofu kuwa michezo ya mapigano ndiyo chanzo cha machafuko lakini alikanusha vikali na kusema ni kama zilivyo fani nyingine na ajira pia kwakua inaweza kuwaingizia washiriki kipato.

Naye Balozi wa Utamaduni wa China nchini Gao Wei alisema wataendelea kushirikiana na chama hicho ili kuhakikisha mashindano hayo yanaendelea kufanyika kila mwaka yakiwa yameboreshwa.

Post a Comment

 
Top