BOIPLUS SPORTS BLOG

MANCHESTER, Uingereza
VIJANA wa Pep Guardiola, Manchester City wamefanikiwa kuwatuliza mashetani wekundu Manchester United kwa mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Old Trafford.

City waliotawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa walifanikiwa kupata bao la kwanza kupitia kwa Kelvin de Bruyne akimalizia kwa ufasaha pasi ya straika wa Nigeria, Kelechi Iheanacho dakika ya 15.

Wakati United wakiendelea kutafuta bao la kusawazisha, Iheanacho ambaye alifunga bao pekee katika mchezo wa kimataifa kati ya Nigeria dhidi ya Taifa Stars aliipatia bao la pili City dakika ya 36 akitazamana na kipa baada wachezaji wengine kudhani ameotea.

Dakika tatu kabla timu hazijaenda mapumziko, Zlatan Ibrahimovic aliipatia United bao la kufutia machozi baada ya kipa wa City kupangua mpira na kumkuta mfungaji.

Kipindi cha pili timu hizo ziliishia kushambuliana tu lakini hakuna aliyeweza kuzifikia nyavu za mpinzani wake.

Kwa matokeo haya City imebaki kileleni kwa kufikisha alama 12 ikifuatiwa na Chelsea yenye pointi 9 sawa na United.


Post a Comment

 
Top