BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
WEKUNDU wa Msimbazi Simba wametoa zawadi ya Eid kwa mashabiki wao baada ya kuigaragaza Mtibwa Sugar kwa  mabao 2-0 katika muendelezo wa ligi ya Vodacom mtanange uliochezwa kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Simba iliuanza mchezo huo kwa kasi ambapo dakika ya tatu walifanya jaribio la kufunga lakini mipango yao ilikwama baada ya safu ya ulinzi ya Mtibwa kuwa makini.

Wekundu hao walitawala karibia dakika zote 45 za kipindi cha kwanza lakini 'Wakata miwa' walitibua mipango yote na kutoruhusu nyavu zao kuguswa kipindi cha kwanza.

Winga Haruna Chanongo almanusura aiandikie Mtibwa bao la kuongoza dakika ya 39 lakini shuti lake lilipanguliwa na mlinda mlango Vicent Agban na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Ibrahim Ajib aliipatia Simba goli la kuongoza kwa kichwa dakika ya 52 baada ya kumalizia mpira wa kona uliopigwa na Shiza Kichuya kufuatia mabeki wa Mtibwa kushindwa kuokoa hatari hiyo.

Laudit Mavugo alifunga goli la pili dakika ya 67 baada ya Mwinyi Kazimoto kuambaa na mpira toka katikati ya uwanja kabla ya kumpasia mshambuliaji huyo raia wa Burundi kipenzi cha mashabiki wa Simba.

Simba iliwatoa Kichuya, Kazimoto na Ajib na kuwaingiza Fredrick Blagnon, Said Ndemla pamoja na Jamal Mnyate huku Mtibwa ikiwapumzisha Stamili Mbonde, Kelvin Idd na Ibrahim Juma na kuwaingiza Saidi Mkopi, Mohamed Juma na Hussein Javu.

Post a Comment

 
Top