BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu
WAGONGA nyundo wa jiji la Mbeya, Mbeya City FC leo wamefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Mbao FC uliochezwa kwenye dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza.

City walikuwa wa kwanza kuziona nyavu za Mbao kwa bao safi la Raphael Daud dakika ya 21 kabla Vicent Philipo hajaisawazishia Mbao katika dakika ya 35.

Kipindi cha pili City walionekana kutulia zaidi huku wakifanya mipango hatari kwa wageni hao wa ligi kuu ambapo dakika ya 55 Omary Ramadhan aliipatia City bao la pili.

Dakika ya 77 krosi kutoka upande wa kulia wa uwanja ilimkuta Omary akiwa peke yake lakini mpira huo ulimgonga na kumkuta Ramadhan Chombo 'Redondo' ambaye aliuweka nyavuni.

Ikiaminika kuwa pambano hilo lingemalizika kwa City kushinda mabao 3-1, mfungaji wa bao la kwanza, Raphael alihitimisha karamu ya mabao baada ya kupachika bao la nne kwa shuti kali akiwa nje ya 18.

Katika michezo mingine ya ligi kuu iliyochezwa leo Mtibwa Sugar imeibamiza Majimaji mabao 2-1, JKT Ruvu imetoka suluhu na African Lyon lakini Kagera wanaongoza bao 1-0 dhidi ya Mwadui zikiwa zimesalia dakika chache.

Post a Comment

 
Top