BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
BAADA ya kutokea uvumi kwenye mitandao ya kijamii, Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF limethibitisha mchezo kati ya Simba na Azam uliokuwa uchezwe Jumamosi ijayo umesogezwa mbele hadi Septemba 24.

Mchezo huo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na wadau wengi wa soka nchini umesogezwa mbele kupisha mechi ya kufuzu michuano ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 kati ya Serengeti boys dhidi ya Congo Brazzaville.

Ofisa Habari wa TFF Alfred Lucas ameiambia BOIPLUS kuwa mchezo huo umesogezwa kwa wiki moja mbele ili kupisha mchezo huo wa timu ya vijana, na endapo wakishinda na kutoka walau sare kwenye mechi ya marudiano watakuwa wamefuzu moja moja katika michuano hiyo itakayofanyika mwakani nchini Madagascar.

"Mchezo kati ya Simba dhidi ya Azam umesogezwa mbele kwa wiki moja kupisha mechi ya vijana, mtanange huo utapigwa Septemba 24" alisema Lucas.

Kwa upande wa timu ya Simba kupitia kwa Msemaji wao Hajji Manara alisema kuwa wao hawawezi kuzungumza chochote kuhusu kusogezwa kwa mchezo huo mpaka watakapo pewa barua na TFF.

"Sisi klabu ya Simba hatujui chochote kuhusu hilo tunasubiri tupewe barua na TFF ndiyo tunaweza kuzungumza lakini kwa sasa hatuna cha kuongea" alisema Manara.

Msemaji wa Wana ramba ramba Azam FC Jaffar Iddi Maganga alisema hata wao wanasikia kwenye mitandao na hawana taarifa rasmi toka TFF wakizipata ndo watajua wafanyaje.

"Ndo tumerudi jana toka jijini Mbeya na leo ni sikukuu kwahiyo tunasubiri barua toka TFF ili tujue tunatoa msimamo gani" alisema Maganga.

Post a Comment

 
Top