BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
UONGOZI wa klabu ya Simba umemshukuru mfanyabiashara Mohamed Dewji 'MO' kwa kutimiza ahadi ya kuwalipa mishahara wachezaji na benchi la ufundi ikiwa ni moja ya ahadi zake kabla ya mchakato wa uwekezaji hisa za asilimia 51 kukamilika.

Dewji maarufu kama MO tayari ameshaanza kulipia mishahara ya wachezaji, benchi la ufundi na Sekretarieti ya klabu na atafanya hivyo katika kipindi chote cha mpito kuelekea mabadiliko ya kimuundo ya klabu ambayo yanaweza kuchukua miezi sita hadi mwaka.

Mbali ya hayo mfanyabiashara huyo mkubwa barani Afrika atalipia kodi ya nyasi bandia na gharama nyingine za uendeshaji wa klabu ikiwa ni miongoni mwa mambo aliyowaahidi Wanasimba wakati akitangaza dhamira yake ya kuwekeza miezi mitatu iliyopita.

Msemaji wa klabu hiyo Haji Manara alisema kuwa uongozi unamshukuru sana MO kwa kutekeleza ahadi zake kwa vitendo hasa katika kipindi hiki ambacho hawana mdhamini yoyote.


"Uongozi wa Simba unamshukuru sana MO, ukizingatia klabu kwa sasa haina mdhamini na unaamini uwekezaji huo ni chachu ya kuwarejeshea furaha wanasimba na hatimae kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom msimu huu na misimu mingine ijayo," alisema Manara.

Aidha Manara amewaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi siku ya Jmosi ya Octoba Mosi  uwanja wa Taifa,kuwashangilia Wekundu hao watakapocheza mechi ya ligi dhidi ya watani zao wa jadi Yanga.

"Tunaamini mechi hiyo ni mwendelezo wa furaha kwa wanachama na washabiki wetu kote nchini kwakua tutaibuka na ushindi.

"Pia tuwaombe sana kukumbuka kununua tiketi kwa mawakala wa Selcom waliopo katika maeneo mbalimbali.
Ikumbukwe tiketi za mechi hii ni za kieletroniki," alimaliza Manara.

Post a Comment

 
Top