BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Dar
LICHA ya kuondokewa na nyota wake wengi wa kikosi cha kwanza msimu uliopita timu ya Mtibwa Sugar bado itaendelea kuleta changamoto kwenye ligi ya Vodacom inayoendelea.

Kauli hiyo imetolewa na kiungo wa zamani wa Wakata miwa hao anayechezea timu ya Simba Muzamir Yassin na kuongeza kuwa wachezaji waliopo ni wazuri wanatakiwa kuaminiwa na kupewa muda ili waendelee kujiamini.

Wakata miwa hao waliondokewa na wachezaji wanne wa kikosi cha kwanza msimu uliopita ambao ni Andrew Vicent 'Dante' aliyejiunga na Yanga huku Muzamir, Shiza Kichuya na Mohamed Ibrahim wakijiunga na Simba.

"Mtibwa bado wana kikosi kizuri wanatakiwa wapewe muda waendelee kuzoeana, wachezaji wengi ni vijana ambao wana uchu wa mafanikio kikubwa ni kuaminiwa," alisema Muzamir.

Aidha kiungo huyo alisema tofauti ya kimfumo kati ya Simba na Mtibwa ndiyo inayofanya ashindwe kufunga magoli na kusaidia kupatikana kwa mengine kama ilivyokuwa wakati akiwa na Wakata miwa.

"Ukiangalia wakati nikiwa Mtibwa kulikuwa na viungo watatu wa kati ambapo mmoja tu ndiye alikuwa na jukumu la kukaba lakini hapa wote tunasaidiana kukaba ndiyo maana sipati nafasi za kufunga," alisema Muzamir.

Kocha wa Simba Joseph Omog amekuwa akiwatumia Jonas Mkude na Muzamir kama viungo wakabaji huku jukumu la kuchezesha timu likikabidhiwa kwa Mwinyi Kazimoto au Said Ndemla.

Kiungo huyo ambaye amejihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Omog alikiri pia kuwa msimu huu ligi ina upinzani mkubwa kutokana na timu nyingi kujiandaa vizuri.

Post a Comment

 
Top