BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu,Dar
HOMA ya pambano la watani wa jadi imezidi kupanda baada ya hii leo kocha msaidizi wa timu ya Yanga Juma Mwambusi kujitokeza hadharani kujinasibu kuondoka na alama zote tatu katika mtanange huo.

Miamba hiyo ya soka nchini yenye mashabiki lukuki itakutana Oktoba mosi katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom utakaopigwa kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam mtanange unaotarajiwa kuvuta hisia za wadau wengi.

Mwambusi ameiambia BOIPLUS kuwa timu yake haipewi nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo kutokana na kiwango wanachokionyesha watani wao Simba lakini amewahakikishia mashabiki wao kuwa 'Mnyama' lazima akae muda ukifika.


Kocha huyo wa zamani wa Mbeya city alisema mechi hiyo wanaichukulia kawaida kama michezo mingine ya ligi na wachezaji wapo kamili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri kwenye mtanange huo.

"Kama kuna watu wanafikiri tutapoteza mechi yetu dhidi ya Simba Oktoba mosi wanajidanganya, mashabiki wetu wasiwe na presha tuna wachezaji wazuri kuliko hao watani wetu muda ukifika kila mtu ataona kitakachotokea" alisema Mwambusi.

Kwa upande wake beki mpya wa mabingwa hao Andrew Vicent 'Dante' ambaye itakuwa mechi yake ya kwanza ya watani wa jadi  alisema kuwa mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na timu zote kujiandaa vya kutosha pamoja na kufanya usajili mzuri ila wao wamejipanga kushinda.


Aidha Dante alisema endapo atapata nafasi ya kucheza katika mechi hiyo atajitahidi kumdhibiti mshambuliaji mpya wa Simba raia wa Burundi Laudit Mavugo asilete madhara kwenye lango lao kutokana na umahiri wa nyota huyo.

Simba inaongoza katika msimamo wa ligi baada ya kujikusanyia alama 13 wakifuatiwa na Yanga wenye pointi 10 huku wakiwa nyuma kwa mchezo mmoja baada ya kushuka dimbani mara nne.

Post a Comment

 
Top