BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Majaliwa Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mechi ya Hisani ya kuchangia maafa ya Kagera kati ya Wabunge wanaoshabikia timu za Simba na Yanga kesho mchezo utakaopigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku kampuni ya Mwananchi Communications na Shirika la Bima ya afya wakimwaga mamilioni.

Mwenyekiti wa Bunge Sports Club ambao ndiyo waratibu wa pambano hilo William Ngeleja alisema maandalizi yote yamekamilika huku vikosi vya timu zote vikiwa vipo kwenye hali nzuri huku akiwahakikishia mashabiki watakaohudhuria burudani ya kutosha.

"Maandalizi yamekamilika lakini naendelea kusisitiza Watanzania waendelee kuchangia hata wasipokuja uwanjani ili tuwasaidie wenzetu waliopatwa na Maafa kwakua matatizo hayana mmoja" alisema Ngeleja.


Mkurugenzi wa Wizara ya Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Alex Nkenyenge alisema katika mtanange huo ambao utatanguliwa na mechi ya Wasanii wa Bongo fleva na Bongo Movies tiketi za Kielectoniki ndiyo zitatumika ili kudhibiti mapato yote yatakayo patikana.

"Tiketi za Kielectoniki ndiyo zitatumika kwenye mchezo huo na kila mchezo utakaofanyika kwenye uwanja huo lazima utaratibu huo ufuatwe," alisema Nkenyenge.

Kuelekea mechi hizo tayari tambo mbali mbali zimeanza ambapo Kocha wa timu ya Bongo Movies William Mtitu ametamba kuwagaraza wapinzani wao huku beki wa kushoto wa Bongo Fleva Rich One akisema kesho watawafunga waigizaji hao bila huruma.

Kampuni mbali mbali zimejitokeza kuchangia ambapo Mwananchi Communication wametoa hundi ya shilingi milioni 10 wakati shirika la bima ya Afya la Taifa NHIF wakitoa hundi ya milioni 5 huku Jubilee Insurance wakichangia milioni 5 pia.

Post a Comment

 
Top