BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
BEKI wa Stand United, Joseph Owino naye amekwenda kufanya majaribio katika timu ya Fanja FC ya Oman ambayo wachezaji wawili wa Tanzania, Mrisho Ngasa na Danny Lyanga wamesajiliwa huko.

Owino ambaye ni raia wa Uganda alisaini mkataba wa mwaka mmoja na Stand United ya mjini Shinyanga ambao una makubaliano ya wazi kuwa endapo atapata timu nyingine ataruhusiwa kuondoka. Fanja wakiridhishwa na kiwango chake basi atavunja mkataba na Stand United.

Owino alithibitisha kuondoka kikosini hapo wakati timu yake kesho Jumapili ikikabiliwa na mechi ngumu dhidi ya Yanga ambayo itachezwa Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.

"Nipo huku kwa ajili ya majaribio naomba mniombee ili nifanikiwe," alisema Owino kwa ufupi.Naye Msemaji wa klabu ya Stand United, Deo Kaji Makomba alisema, "Ni kweli ametuaga kuwa anakwenda kwenye majaribio, hivyo tunamuombea afanikiwe."

Ngassa amejiunga na timu hiyo baada ya kuvunja mkataba na Free State Stars ya Afrika Kusini huku Lyanga naye akiuzwa na Simba baada ya kukosa nafasi kwenye kikosi cha Joseph Omog. Wachezaji wote wawili wamesaini mkataba wa miaka miwili kila mmoja.

Post a Comment

 
Top