BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
KLABU kongwe nchini ya Pan African inatarajia kufanya mkutano mkuu wa wanachama Jumapili Septemba 11 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kurudisha umoja.

Pan African ilitikisa miaka ya nyuma katika mchezo wa mpira wa miguu lakini migogoro ya mara kwa mara ndiyo chanzo cha kuwapoteza wakongwe hao kwenye ramani ya soka.

Mwaka 2007 ndiyo walishiriki ligi kuu kwa mara ya mwisho lakini mvutano ndani ya klabu uliopelekea hadi viongozi kupelekana mahakamani ukavuruga taswira ya timu na kuporomoka hadi ligi daraja la pili ngazi ya Mkoa.

Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye ofisi za Baraza la Michezo Tanzania Katibu mkuu wa Klabu hiyo Saad Matheo alisema dhamira ya mkutano huo ni kurudisha umoja uliopotea kwa muda mrefu ili kurejesha makali ya wakongwe hao.

"Nia yetu ni kurudisha umoja ndani ya klabu ambapo tutaiandaa vizuri timu yetu ili kuipandisha kucheza ligi kuu," alisema Matheo.

Aidha Matheo alisema pia katika mkutano huo watapokea wanachama wapya na endapo watawahi basi watasajiliwa na kuruhusiwa kushiriki moja kwa moja kwa kuchangia mawazo wakati mkutano huo ukiendelea.

Kwa sasa klabu hiyo kongwe ina wanachama 75 pekee ambapo awali walikuwa wanazidi mara tatu ya idadi iliyopo.

Post a Comment

 
Top