BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
TIMU ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 Serengeti Boys imeibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Congo Brazzaville kwenye mchezo wa kwanza wa kufuzu michuano ya Afrika kwa vijana uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo ambao mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Habari Michezo Sanaa na Utamaduni Nape Nnauye ambapo mashabiki waliruhusiwa kuingia bure kwa ajili ya kutoa sapoti kwa vijana wa Serengeti ulianza kwa kasi huku timu zote zikishambuliana kwa zamu lakini wageni walionekana kutulia zaidi.


Dakika ya 14 Congo walifanya shambulizi kali langoni mwa vijana wa Serengeti ambapo kiungo Langa-Lesse Percy alipiga shuti akiwa ndani ya 18 na kugonga mwamba wa chini kabla ya kuokolewa na mabeki.

Mshambuliaji Yohana Oscar alifunga magoli mawili ndani ya dakika tatu (38 & 41) baada ya Serengeti kushambulia lango la wageni kama nyuki ambapo wangeweza kupata goli la tatu kama wangeongeza umakini.

Kipindi cha pili Congo walirudi kwa kasi huku wakionesha dhamira ya kurudisha mabao lakini golikipa Ally Hussein wa Serengeti alikuwa makini langoni.

Percy iliwapatia wageni goli la kwanza dakika ya 73 kwa mkwaju wa penalti baada ya Israel Patrick kumfanyia madhambi mchezaji mmoja wa Congo.


Dakika ya 81 'Super Sub' Issa Abdi aliipatia Serengeti goli la tatu baada ya mabeki wa Congo kushindwa kuokoa mpira wa kona iliyopigwa na Asadi Juma kabla ya kumkuta mfungaji huyo.

Bopoumela Chardon aliipatia Congo goli la pili dakika ya 90 baada ya wachezaji wa Serengeti kushindwa kuondoa mpira wa kona uliokua unazagaa langoni.

Serengeti iliwatoa Ibrahim Abdallah, Oscar na Ramadhani Kambili na kuwaingiza Muhsin Makame, Makamba na Kelvin Kayego. Congo iliwapumzisha Mantourari Aldo,Mboungou Prestige na Kiba Konde na kuwaingiza Mokouana Beni, Chardon pamoja na Mountou Edward.

Post a Comment

 
Top