BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
SERIKALI imeagiza Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa hesabu za Serikali 'CAG' kufanya ukaguzi wa Rasilimali watu na fedha katika Shirikisho la mpira wa Miguu Tanzania TFF ili kupunguza minong'ongono ya wizi wa fedha.

Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Nape Nnauye amefanya ziara ya katika ofisi za TFF na kuagiza CAG kufanya ukaguzi ili kupunguza dhana ya kupotea fedha kinyume na utaratibu.

Waziri Nape pia alitaka kupata ufafanuzi juu ya kuwepo kwa madai ya baadhi ya watumishi ambao wanadai misharaha yao iliyolimbikizwa kwa muda mrefu.

"Nimemwagiza CAG kufanya ukaguzi wa rasilimali watu na fedha za TFF ili tujiridhishe na kuondoa wasiwasi miongoni mwa wadau wa soka" alisema Waziri Nape.

Akijibu tuhuma za watumishi kutolipwa fedha zao za mishahara Rais TFF Jamal Malinzi alisema mfumo mpya unaotumiwa na FIFA kugawa fedha umechelewa ndiyo maana imejitokeza hali hiyo ila suala hilo litafanyiwa kazi na watalipwa fedha zao muda wowote kutoka sasa.

"Tatizo ni mfumo mpya unatumiwa na FIFA kwa sasa ila muda si mrefu watumishi wote watalipwa mishahara yao,"alisema Malinzi.

Wakati huo huo Waziri Nape imeitaka Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwa makini na uchaguzi mkuu wa Shirikisho hilo utakaofanyika mwakani ili kuziba mianya yote ya Rushwa ili kuwapata viongozi bora.

Post a Comment

 
Top