BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Dar
LICHA ya ushindani mkubwa uliopo kwenye ligi kuu kwa sasa bado vijana wa Mwadui FC wamejipanga kuchukua ubingwa.

Kauli hiyo inaweza ikaonekana kama kichekesho kwa mashabiki wengi wa soka nchini lakini mikakati waliyojiwekea Wachimba madini hao ndio inayowapa kiburi cha kutamba kunyakua taji la ubingwa mwaka huu.

Akizungumza na BOIPLUS kiungo wa timu hiyo Abdallah Seseme ameonyesha kuunga mkono kauli ya kocha Jamhuri Kihwelo 'Julio' kuwa pamoja na timu nyingi kujiandaa vizuri na ligi bado jambo hilo haliwezi kudhoofisha dhamira yao ya kunyakua msimu huu.

"Katika maisha ukitaka kufanikiwa lazima ujiwekee malengo, na sisi kama timu tumeweka mikakati ya kuhakikisha tunachukua ubingwa," alisema Seseme.

Akizungumzia mchezo wao wa wikiendi dhidi ya mahasimu wao Stand United Seseme alisema mechi itakuwa ngumu hata kama wapinzani wao wapo kwenye mgogoro wa kiuongozi.

"Mechi itakuwa ngumu sana kwakua sisi ni mahasimu lakini tuna nafasi ya kuibuka na ushindi kwakua mashabiki wetu wengi watajitokeza kutupa nguvu," alisema Sesemi.

Post a Comment

 
Top