BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu
BAADA ya mechi yao dhidi ya Yanga kupigwa kalenda Maafande wa JKT Ruvu wamehamishia hasira zao kwenye mchezo na African Lyon utakaochezwa  Jumamosi Septemba 3 katika uwanja wa Mabatini Mlandizi mkoani Pwani.

Katika mchezo uliopita dhidi ya Simba Ruvu ilicheza vizuri hasa safu ya ulinzi huku mlinda mlango Saidi Kipao akionekana kikwazo kwa Washambuliaji wa Wekundu hao kufunga magoli.

Maafande hao wanaendelea na mazoezi kwenye uwanja wa JKT Mbweni kuwavutia kasi Lyon ambao wikiendi iliyopita ilikubali kichapo cha mabao 3-0 toka kwa mabingwa watetezi timu ya Yanga.

Msemaji wa Maafande hao Afisa Mteule daraja la pili Constantine Masanja alisema kuwa kikosi chao kinaendelea vizuri na mazoezi huku wachezaji wakiwa na ari ya kuibuka na ushindi katika uwanja wao wa nyumbani.

Masanja alisema pia kuwa wachezaji wao wanne waliokuwa wakishiriki michuano ya majeshi watajiunga na kambi hiyo muda wowote kutoka sasa baada ya kumalizika kwa mashindano hayo.

"Kikosi kiko vizuri Wachezaji wana morali ya kutosha na wameahidi ushindi katika uwanja wetu wa nyumbani ili tujiweke sehemu salama kwenye msimamo wa ligi," alisema Masanja.

Kikosi hicho kwa sasa kinanolewa na kocha Malale Hamsini ambaye msimu uliopita alikuwa akiifundisha Ndanda FC ya mkoani Mtwara.

Post a Comment

 
Top