BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda, Dar
Kikosi cha Simba kilichofungwa mabao 2-0 na Yanga Februari 20

 ILIKUWA miezi, siku hatimaye sasa tunahesabu masaa tu vigogo wa soka nchini Tanzania Simba na Yanga wavaane katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom hapo kesho.

Mara ya mwisho timu hizi kukutana ilikuwa Februari 20 ambapo mabingwa watetezi Yanga waliibugiza Simba mabao 2-0 a kufanikiwa kuwapoteza kabisa kwenye mbio za ubingwa.

Kesho timu hizo zitakutana mambo yakiwa tofauti kabisa, kwanza Simba inaongoza ligi ikiwa na alama 16 huku Yanga ikishika nafasi ya tatu kwa pointi zao 10. Lakini kingine, Simba hii ni kama mpya kabisa ukilinganisha na ile iliyopigwa mabao 2-0.

Ukitazama kikosi cha kwanza cha Simba msimu huu utagundua kuna wachezaji wapya takribani watano ambao hawakuwepo kwenye 'Kariakoo Derby' iliyopita. Hawa ni pamoja na Janvier Bukungu, Method Mwanjali, Muzamiru Yassin, Shiza Kichuya na Laudit Mavugo. Lakini pia kukiwa na wapya wengine kadhaa katika benchi.


Kikosi cha Yanga kilichoifunga Simba mabao 2-0 mwezi Februari.

 Hii ni tofauti kabisa na kikosi cha Yanga ambacho hakijatetereka hata kidogo. Kuna uwezekano mkubwa mabadiliko ya kile kilichoshinda mchezo uliopita yakawa machache mno kuelekea mechi hii yenye msisimko wa kipekee.

Wachezaji pekee wa kikosi hiki (pichani) ambao wanaweza wasiwepo kwenye kikosi cha kwanza kwa ajili ya mchezo wa kesho ni Pato Ngonyani na Haruna Niyonzima ambaye mechi nyingi za msimu huu amekuwa akianzia benchi, lakini wanaobaki wote wana nafasi kubwa ya kuanza.

Ukiachilia mbali suala la uchovu ambao wachezaji wa Yanga wanao kutokana na kucheza mechi nyingi za ndani na nje, bado jambo la kutokuwa na mabadiliko makubwa kwenye kikosi chao linabaki kuwa silaha yao kuu. Wachezaji hawa wamezoeana tofauti na wale wa kikosi cha Simba ambao wengi ni wapya na bado hawajatengeneza muunganiko mzuri.

Hapa ni sawa na kusema "Simba mpya inaenda kupambana na Yanga ya zamani". Dakika 90 ndizo zitakazotoa jibu. 

Post a Comment

 
Top