BOIPLUS SPORTS BLOG

GENK, Ubelgiji
Picha inayoonyesha mguu wa Samatta akipatiwa matibabu

IKICHEZA bila straika wake tegemeo Mbwana Samatta, klabu ya KRC Genk leo imeshindwa kuutumia vizuri uwanja wake wa nyumbani wa Cristal Arena baada kukubali kichapo cha mabao 2-0 toka kwa Anderlecht.

Samatta alipata maumivu ya goti katika mchezo wa kombe la Europa dhidi ya Rapid Wien ambapo Genk walipoteza kwa mabao 3-2.

Akizungumza na BOIPLUS kutokea mjini Genk Samatta amesema alishindwa kufanya mazoezi na wenzake kutokana na maumivu hayo na kwamba sasa anapatiwa matibabu ili arudi kuitumikia klabu hiyo inayoshika nafasi ya tisa katika msimamo wa ligi kuu nchini Ubelgiji kwa kujikusanyia pointi 10.

"Niliumia ile mechi ya Europa ndio sababu leo hata benchi sikukaa, ila naendelea kupata matibabu mazuri na naamini nitakuwa poa hivi karibuni," alisema Samatta.

Katika mchezo wa leo mabao ya Anderlecht yalifungwa na washambuliaji Kara Mbodji na Harbaoui katika dakika za 64 na 76 huku nyota wawili wa Genk, Pozuelo na Omar Colley wakitolewa nje kwa kadi nyekundu.

Post a Comment

 
Top