BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu,Dar
STRAIKA  wa kimataifa wa Yanga, Amissi Tambwe ambaye msimu uliopita alikuwa mfungaji bora ametamba kuwa hata msimu huu bado ana nafasi kuchukua tena licha ya kuwa  na ushindani mkubwa kutoka kwa washambuliaji wengine akiwemo mburundi mwenzake anayekipiga na Simba, Laudit Mavugo.

Nyota huyo wa zamani wa Simba  aliweka rekodi ya ufungaji msimu uliopita kwa kufumania nyavu mara 21 huku msimu huu akiwa tayari ameshafunga mabao matatu baada ya kushuka dimbani mara nne.

Akizungumza BOIPLUS Tambwe alisema kutoka na ushindani uliopo sasa hivi atajitahidi kuhakikisha anatumia kila nafasi kufunga ili kujihakikishia kutetea tuzo hiyo ambayo mpaka sasa amechukua mara mbili akiwa na timu za Simba na Yanga.


“Ushindani umeongezeka sana, hivyo nitatumia  kila nafasi nitakayoipata uwanjani  kufunga ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuandika historia ya kuchukua ufungaji bora kwa mara pili mfululizo nikiwa na timu yangu hii ya Yanga,"alisema Tambwe.

Tambwe ambaye yupo mkoani Shinyanga na timu yake anatarajiwa kuwepo kwenye kikosi kitakachoshuka dimbani kumenyana na Stand United Jumapili ijayo ambapo amepania kucheka na nyavu kila atakapopata nafasi.

Tambwe ametengeneza ushirikiano mzuri na mshambuliaji Donald Ngoma ambapo msimu uliopita ndiyo ilikuwa kombinesheni iliyozalisha mabao mengi katika ligi nzima.

Post a Comment

 
Top