BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, Shinyanga
MABAO ya washambuliaji wa Yanga Amiss Tambwe na Donald Ngoma yameiwezesha timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mwadui na kuzima tambo za kocha Jamhuri Kihwelo 'Julio' ambaye alijinasibu kuibuka na ushindi.

Mchezo huo wa Ligi kuu ya Vodacom uliopigwa kwenye dimba la CCM Kambarage ulikuwa ni wa kasi huku timu hizo zikishambuliana kwa zamu ingawa umakini katika umaliziaji ulizinyima mabao timu hizo.

Yanga walijipatia bao la kwanza katika dakika ya tano tu baada ya Tambwe kumalizia kirahisi mpira ulioachwa ukizagaa jirani kabisa na lango la Mwadui huku mabeki na Kipa wakishikwa na kigugumizi.

Mechi hiyo ulishuhudia wachezaji Thaban Kamusoko na Said Nassor 'Cholo' wakitolewa nje baada ya kupata maumivu na kushindwa kuendelea na mchezo huo uliokuwa wa nguvu na kukamiana.

Kipindi cha pili timu zote zilipata nafasi kadhaa ambazo walishindwa kuzitumia hadi dakika 90 za kawaida zilipomalizika kabla mwamuzi wa mezani hajaonyesha dakika za nyongeza.

Ikionekana kwamba mchezo huo ungemalizika kwa matokeo ya bao 1-0, tena mashabiki wengi wakiwa wameshainuka vitini kutoka uwanjani, krosi ya kiungo Haruna Niyonzima aliyeingia badala ya Kamusoko ilitua kichwani kwa Ngoma na kufunga bao la pili.

Post a Comment

 
Top