BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu
MDHAMINI wa Stand United ambye ni Kampuni ya uchimbaji Madini nchini Acacia amevunja mkataba wa kuidhamini timu hiyo huku wachezaji wakishindwa kuelewa nani atawalipa mishahara pamoja na fedha zao za usajili.

Stand United iliingia mkataba na Acacia wa miaka miwili tangu msimu wa mwaka jana kwa kitita cha Sh 2.4 bilioni ambapo tayari mwaka mmoja umemalizika. 

Mapema mwezi uliopita Acacia walitoa notisi ya miezi mitatu ili wawe wamemaliza mgogoro wao unaoitafuna timu hiyo kati ya pande mbili Klabu na Kampuni, mgogoro ambao umeonyesha kuwakera wadhamini hao na kuamua kujiondoa.

Akizungumza na BOIPLUS nahodha wa timu hiyo, Jacob Masawe alisema kuwa wamechanganywa juu ya kujitoa kwa mdhamini huyo kwani wachezaji hawajapata haki zao ikiwemo mishahara na pesa za usajili.

"Hatujui hatma yetu ni ipi maana hata pesa za usajili kwa wachezaji waliosajiliwa na walioongeza mikataba hakuna aliyelipwa ikiwemo mishahara, Acacia wajaribu kufikiria juu ya malipo hayo, watulipe halafu waendelee na taratibu zao.

"Kiukweli huu unaweza ukawa ndiyo mwanzo wa Stand kuanza kufanya vibaya bora hata pesa za usajili zingelipwa, usishangae hata baadhi ya wachezaji kuondoka maana tutaishije," alisema Masawe.

Kwa upande wa Acacia, mkuu wa kitengo cha uhusiano na mawasiliano, Nector Foya alisema, "Kuna mambo hayakutekelezwa katika ule mkataba wa mwaka mmoja kwa maana ya msimu uliopita lakini pia mgogoro unaondelea ndani ya klabu hiyo ndiyo maana tumeona ni vyema tuvunje mkataba. 

"Kuna baadhi ya mambo tutayaweka sawa ikiwemo kuwalipa mishahara ya miezi mitatu kuanzia Agosti hadi Oktoba, mshahara wa Julai tulilipa ila kuhusu usajili hilo ni suala la uongozi wa klabu ikiwemo malipo ya kocha Patrick Liewig," alisema Nector.

Katibu mkuu wa Stand United, Kennedy Nyangi alisema, "Hapa tutajipanga kuona jinsi gani ya kuendesha timu na ni kweli hakuna mchezaji aliyelipwa pesa ya usajili na wanadai mishahara ambayo tunaamini watalipa kwa mujibu wa utaratibu wa uvunjaji mkataba," 

Habari zaidi zinasema kwamba Liewig aliomba pesa ya usajili Sh 80 milioni lakini Acacia walitoa ofa kwamba usajili usizidi Sh 100 milioni ingawa pesa hizo hazijatolewa hadi leo.

Post a Comment

 
Top