BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
MSHIKE MSHIKE wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara  unatarajiwa kuendelea tena kesho Jumamosi ambapo nyasi za viwanja sita zitakuwa shakani baada ya miamba 12 kushuka dimbani kutafuta pointi tatu muhimu.

Macho na masikio ya wadau wengi wa soka yatakuwa kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam ambao Azam wataikaribisha Simba katika mtanange unaotabiriwa kuwa mzuri kutokana na miamba hiyo kulingana pointi huku wakiwa wamecheza michezo sawa.

Vikosi vya timu zote mbili vinaonekana vipo kwenye ubora wa juu kutokana na kandanda safi wanalotandaza hali inayofanya mchezo huo uwe na mvuto zaidi.

Azam walitaka mchezo huo ufanyikie kwenye uwanja wao wa Azam Complex lakini Shirikisho la miguu Tanzania TFF likawagomea na kusema dimba hilo haliwezi kuchukua mashabiki wengi wa Wekundu hao hali iliyozusha mvutano kabla yakufikia mapatano ambapo sasa mtanange huo utapigwa kwenye uwanja wa Uhuru.

Mchezo mwingine unaosubiriwa kwa hamu ni wa mabingwa watetezi wa kombe hilo timu ya Yanga ambao wamesafiri hadi mkoani Shinyanga kuwakabili Wachimba madini timu ya  Mwadui FC ambao wamepania kuwatoa nishai vijana hao wa Jangwani.


Yanga wamesafiri na kikosi chao chote cha wachezaji 26 ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mchezo huo huku wenyeji wao wakiapa kuwaangamiza kwenye uwanja wa Kambarage mkoani humo.

Mechi nyingine yenye mvuto wa aina yake utakuwa kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ambapo Tanzania Prisons watakuwa wenyeji wa Mbeya City ( Mbeya Derby) ambapo kwa kawaida mtanange huo huwa gumzo wiki mbili kabla ya kupigwa rasmi dimbani.

Kwenye uwanja wa Manungu mkoani Morogoro Mtibwa Sugar itawakaribisha ndugu zao Kagera Sugar ambapo kocha Meck Mexime atakanyaga kwenye dimba hilo baada ya kuachana nao ulipomalizika msimu uliopita hali inayoongeza chachu ya mtanange huo.


Mchezo mwingine wa kesho, Ruvu Shgooting itakuwa mwenyeji wa Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani wakati Keshokutwa Stand United ya Shinyanga itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa CCM Kambarage.

Mzunguko wa tano wa ligi hiyo utafungwa kwa mchezo kati ya African Lyon  dhidi ya Toto African kwenye Uwanja wa Uhuru,Jumanne Septemba 20.

Post a Comment

 
Top