BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda
KIPINDI cha kwanza cha mchezo kati ya Nigeria na Taifa Stars kimemalizika kwa timu hizo kwenda vyumbani bila kufungana. Haya hapa ni yaliyojiri.

MANULA 'Man Of The 45 Minutes'
Kama si uhodari wa kipa Aishi Manula tungeshuhudia Stars ikienda mapumziko ikiwa nyuma kwa mabao yasiyopungua manne. 

Manula akionyesha kujiamini huku akiwa makini mno alifanikiwa kuokoa michomo kadhaa iliyokuwa ikielekea langoni mwa Stars baada ya walinzi kuzidiwa ujanja na washambuliaji wa Nigeria wanaoongozwa na Victor Moses.

KAMA SI KUVURUGWA BASI NIGERIA HAWAKUWA NA BAHATI
Achana na michomo aliyookoa Manula, Nigeria wametengeneza nafasi za mabao zisizopungua 10 lakini zaidi ya 50% ya nafasi hizo washambuliaji wake wamepiga mipira ya ajabu isiyo na madhara.

Mara kadhaa mipira imepaa na kutoka nje ya lango huku pia ikiwagonga kama watoto wanaojifunza kucheza soka.

LICHA YA KUSHAMBULIWA, STARS WAMETULIA TULII
Hakuna mchezaji anayeonyesha kupagawa, nyota wa Tanzania wameonyesha ukomavu mkubwa licha ya presha kubwa ya mchezo huo. 

Walinzi Andrew Vicent, David Mwantika, Shomari Kapombe na Mohamed Hussein wamejitahidi kutuliza akili mchezoni na kuzuia baadhi ya mashambulizi.

Wakati huo huo viungo Himid Mao na Jonas Mkude wamekuwa wakishuka chini kabisa kuongeza nguvu kwenye safu hiyo iliyoandamwa na mashambulizi.

WASHAMBULIAJI WAMENYIMWA NAFASI YA KUONYESHA 'WALIYONAYO' MIGUUNI
Kitendo cha Nigeria kuwashambulia Stars muda wote kimewafanya mastraika wa Stars waishie eneo la kati ya uwanja ili kusaidia kupokonya mipira badala ya kusogea katika eneo la hatari la Nigeria. 

Mbwana Samatta alipata nafasi moja ambayo alishindwa kuitumia hadi alipoangushwa lakini refa 'akapeta'. John Bocco amekuwa akipambana na walinzi wa Nigeria lakini eneo analocheza limekuwa kikwazo kwake kuleta hatari hata pale anapofanikiwa kupokonya mipira. 

Post a Comment

 
Top