BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu ,Dar
KIKOSI cha Mabingwa wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara timu ya Yanga kinaondoka hii leo kuelekea mkoani Mtwara tayari kwa mchezo wao dhidi ya Ndanda FC utakaofanyika kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona keshokutwa Jumatano.

Yanga inaondoka ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-0 walioupata dhidi ya African Lyon kwenye mechi yake ufunguzi baada ya kutolewa kwenye michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika.

Kocha msaidizi wa timu hiyo Juma Mwambusi ameiambia BOIPLUS kuwa wanatakiwa kuendelea kupata ushindi zaidi katika michezo yao ya mwanzoni ili Wachezaji waendelee kujiamini wakiwa uwanjani.

Mwambusi alisema pia wachezaji wao wana morali ya kuibuka na ushindi kwenye mtanange huo licha ya wapinzani wao kujipanga ili kuondoka na alama zote kwenye uwanja wao wa nyumbani.

"Tumejipanga kuhakikisha tunaendelea kupata matokeo ya ushindi kwenye kila mchezo, Wachezaji wana morali nzuri na wametuahidi ushindi kwenye mechi yetu ya kwanza ya ugenini," alisema Mwambusi.

Kocha huyo wa zamani wa timu ya Mbeya city alisema ligi ya msimu ni ngumu kulinganisha na misimu iliyopita kutokana na timu nyingi kujipanga vizuri huku akikiri ugumu wa kutoka na ushindi kwenye viwanja vya ugenini.

"Msimu huu utakuwa mgumu sana na kupata ushindi kwenye uwanja wa ugenini itakuwa shida zaidi lakini sisi kama mabingwa watetezi tumejipanga kukabiliana nao," alimalizia Mwambusi.

Post a Comment

 
Top