BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
KATIKA hali inayoonekana kupania kuondoka na alama zote tatu kwenye mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Mwadui FC mabingwa watetezi Yanga wamesafiri na wachezaji wote 26 waliowasajili msimu huu.

Yanga imesafiri asubuhi ya leo kuelekea jijini Mwanza kwa usafiri wa ndege ya Fastjet kabla ya kwenda mkoani Shinyanga tayari kwa mtanange huo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi soka nchini.

Kiongozi mmoja wa mabingwa hao ambaye hakutaka kutajwa jina kwenye mtandao huu alisema kocha Hans van Pluijm anawaheshimu wapinzani wao ndiyo maana akaondoka na silaha zake ili kujihakikishia kurudi na pointi zote.

"Kikosi chetu kimeondoka na wachezaji wote 26 tuliowasajili msimu huu na benchi la ufundi ili kuhakikisha tunaibuka na alama zote tatu kwenye mchezo wetu dhidi ya Mwadui"

"Wachezaji Kelvin Yondani, Malimi Busungu na Gofrey Mwashiuya walishindwa kushiriki baadhi ya mechi kutokana na sababu mbali mbali lakini kwa sasa wako vizuri na wamejumuishwa kwenye kikosi kilichosafiri na timu" alisema kiongozi huyo.

Mapema wiki hii kocha wa Mwadui Jamhuri Kihwelo Julio' alinukuriwa akisema kuwa mchezo wao dhidi ya mabingwa hao wamejipanga kushinda tena kwa idadi kubwa ya mabao kwenye dimba la CCM Kambarage hali iliyowatisha Yanga kubeba silaha zake zote.

Yanga ina alama 7 baada ya kushuka dimbani mara tatu akizidiwa pointi tatu na vinara Azam ambao wako sawa na Simba wakitofautiana magoli ya kufunga na kufungwa.

Post a Comment

 
Top